Mizunguko yako inaweza kuwa na madhara katika utoaji wa kabondaioksaidi itokanayo na mafuta. Kwenye orodha hapo chini, vya juu ni nzuri zaidi kwa mazingira, na vya chini ni mbaya zaidi kwa mazingira:

Usiende, au ikibidi, usiende mbali au usiende mara nyingi! Mfano jiulize kama kikao hicho cha kazi kinaweza kufanyika kirahisi kwa simu ya video kama tu kukutana? Vikao kupitia video vinazidi kuwa na ufanisi siku hadi siku, na uzuri tuna huduma nzuri ya intaneti hapa Daresalaam. Kwa burudani fikiria kuhusu kuchagua zile ambazo zinapatikana karibu, kama fukwe zetu nzuri za Daresalaam, au vivutio vyetu vilivyopo Tanzania na Kenya ambavyo huweza kufikika kwa meli au basi. Kama utasafiri, jaribu kusafiri mara chache, na kila baada ya muda mrefu, kuliko safari za mara kwa mara.

Tembea/kimbia! Kwa umbali mfupi mfupi, jaribu tu kwenda kwa kutembea au kukimbia, utaimarisha ukakamavu kila siku kwa mazoezi, na pia kurahisisha usafiri wakati huo huo!

Endesha baiskeli! Uendeshaji wa baiskeli ni njia muhimu ya kuzungukia mji wa Dar, na pia unaimarisha ukakamavu wako kupitia usafiri huu, huhitaji kwenda gym. Jiunge na jamii ya waendesha baiskeli Daresalaam UWABA. Miundombinu ya uendeshaji wa baiskeli inaimarika kwa kupata barabara nyingi za pembeni za kuhudumia barabara kuu (service roads), na njia za waendesha baiskeli, kama hautaki kutumia barabara kubwa. Barabara nyingi ndogo zina matuta, au barabara tu za changarawe, ambazo pia zinasaidia kupunguza mwendokasi na hatari. Daresalaam ni tambarare (hakuna miinuko sana), ambapo hilo linafanya kuwa eneo zuri kwa uendeshaji wa baiskeli. Hali ya hewa yetu, haswa asubuhi na jioni kabla jua kuzama, ni nzuri kwa uendeshaji wa baiskeli. Ukiwa mwendesha baiskeli tu unakuwa VIP (mheshimiwa) ambapo unaweza kuipita misongamano mingi barabarani. Ukiwa na baiskeli Dar, kuna mara nyingi sana utafika haraka kuliko hata mwenye gari/vyombo vya moto. Ukitaka usifike na majasho, unaweza kubeba nguo za kubadilisha na unaweza kuuliza watu wa uendako kama kuna bafu na vifaa vya kuogea (mfano kazini); kama hamna, unaweza kuomba waweke! Kama hata ukiuliza maaskari/walinzi kwenye majengo, wanaweza kukuelekeza sehemu ilipo huduma ya bafu, au hata bafu rahisi za kutumia ndoo, ambapo unaweza usipajue.

Tumia huduma ya usafirishwa wa bidhaa kwa baisikeli! Fasta Cycle Messengers ndio pekee wasiotumia vyombo vya moto kwa huduma za kusafirishwa bidhaa – simu yao 0714132782 (07141FASTA). Wanaweza hata kukufanyia manunuzi na kuleta bidhaa zako nyumbani, kama huna muda.
Treni ni moja kati ya vyombo vya moto vinavyotoa kabondaioksaidi kidogo zaidi. Daresalaam – Dodoma sasa inajengwa njia ya treni (garimoshi) la mwendokasi – inatarajiwa kukamilika ndani ya kama mwaka hivi. Ikikamilika ni matumaini safari za ndege katika Dar na Dodoma zitapungua. Pia kuna treni za Dar kwenda Zambia (TAZARA), Dar kwenda Kigoma au Mwanza kupitia Dodoma, na sasa pia treni kutoka Dar mpaka Moshi imeanza tena. Inatumainiwa hili litaboreshwa kadiri Tanzania itavyowekeza zaidi katika reli.

Basi ni aina ya usafiri unaotoa kabondaioksaidi kidogo, kwasababu uchafuzi hewa wa watu 50 wanaotumia basi moja ni mdogo kuliko watu 50 wanaosafiri katika magari mengi.
Basi ndani ya Daresalaam- tuna mabasi mazuri na ya kisasa ya mwendokasi (DART) yanayotoa huduma kati ya Kivukoni, Gerezani, njia panda ya Morocco na kufuata barabara ya Morogoro kwenda Ubungo/Kimara/Mbezi, ambayo pia yametanuliwa kuelekea maeneo mengine (mzunguko mpya). Pia tumebahatika na usafiri wa kutosha na mara kwa mara kwa daladala, ambazo zinaenda kila kona ya jiji na huwezi kusubiri muda mrefu. Daresalaam ina aina mbalimbali za usafiri, na usafiri wa mara kwa mara wa mabasi kulinganisha na majiji mengine duniani! Tafiti kuhusu mizunguko yako ya ndani ya jiji na usafiri wa basi, kwa kuuliza watu na kujaribu kuutumia.

Basi kwa safari za mbali/mikoani – Tanzania pia ina mtandao mzuri wa mabasi ya mbali/mikoani ambayo ni mazuri, na usalama ukiwa umeboreshwa vizuri kwa miaka ya karibuni iliyopita. Kwa usafiri wa mikoani, matumizi ya mabasi yawe ndo kipaumbele chako!
Meli/Usafiri wa majini – Meli kwenda Zanzibar kunatoa kabonidaioksaidi kidogo kuliko kuruka kwa ndege kwenda Zanzibar. Uendapo Zanzibar – tumia meli!

Pikipiki na bajaji – Unaweza kuzunguka Daresalaam vizuri kwa pikipiki/bodaboda na bajaji, ambazo hutumia mafuta kidogo kuliko magari binafsi.
Magari binafsi – Magari yana utoaji wa kabonidaioksaidi mkubwa zaidi kwa mtumiaji kulinganisha na aina nyingine zote za usafiri hapo juu. Inawezekana kabisa kuishi Daresalaam bila kumiliki gari, na utajiokolea gharama za kununua, kodi, bima, marekebisho, gharama za mafuta, gharama za kupaki na kutumia muda mwingi kwenye misongamano, kama huna gari! Magari hutumia nishati katika kuyatengeneza na kutumia. Kama ni lazima kutumia gari fikiria kama linaweza kutumika na watu wengi kuliko kila mtu kupanda gari tofauti – jadiliana na wanafamilia wako, majirani, wanafunzi wenzio na wafanyakazi wenzio kuhusu kushea usafiri. Huduma za usafiri wa kushea kama Uber na Taxify unaleta maana zaidi kwani wakati dereva amekufikisha anaweza kumchukua abiria mwingine na haitakuwa utoaji wa hewa chafu pasipokuwa na ulazima, kama akirudi na gari kavu kituoni. Unaweza kumudu safari nyingi zaidi za usafiri wa kukodi kila unapohitaji, kwa gharama za kununua na kulihudumia gari!
Usitumie ndege/ punguza kusafiria kwa ndege! Usafiri wa anga ni aina ya usafiri ambao unaongoza kutoa hewa chafu hata tukihesabia kwa kila abiria kwa kilomita. Kama hujawahi kupanda ndege – hongera sana – hujaacha nyayo za kabonidaioksaidi kama ambao wamewahi. Kupunguza safari za anga inaweza kuwa suluhisho lenye ufanisi zaidi la kupunguza nyayo zako za kaboni. Jitahidi kuwa na safari chache za kwenda mabara mengine, haswa kwa biashara/kazi – fikiria kuhusu vikao vya kutumia video na webinars badala yake. Ndani ya bara la Afrika – usafiri wa gari ni bora kuliko wa ndege, na usafiri wa mabasi ni bora kuliko gari za kawaida. Kwa starehe mwendo wa polepole (“slow travel”) ina maana kuwa utajionea vizuri maeneo unayotembelea kuliko kuyapita kwa haraka na ndege.
Ukurasa unaofuata: Nyumba na nishati
Tovuti hii imeundwa na Elaine mwaka 2019. Wasiliana na mimi kwa Mastodon kama utapenda kusaidia kusasisha tovuti hii mastodon.ie/@ElaineActivism . Kama huna akaunti ya Mastodon, unaweza kujiunga hapa mastodon.social
